1 Wakorintho
Mlango 13
 1 Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
2  Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
3  Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.
4  Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
5  haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
6  haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
7  huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
8  Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.
 9  Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;
 10  lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.
 11  Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.
 12  Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.
 13  Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.