Habakuki
Mlango 3
 1 Sala ya nabii Habakuki.
2  Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.
3  Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake.
4  Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake.
5  Mbele zake ilikwenda tauni, Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.
6  Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.
7  Naliziona hema za Kushani katika taabu; Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.
8  Je! Bwana aliikasirikia mito? Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito, Au ghadhabu yako juu ya bahari, Hata ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu?
 9  Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito.
 10  Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake.
 11  Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.
 12  Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu; Ukawapura mataifa kwa hasira.
 13  Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani.
 14  Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe; Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya; Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri.
 15  Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako, Chungu ya maji yenye nguvu.
 16  Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka, Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile; Ubovu ukaingia mifupani mwangu, Nikatetemeka katika mahali pangu; Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki, Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.
 17  Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;
 18  Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.
 19  YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.