Ezekieli
Mlango 31
 1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno 
la Bwana likanijia, kusema,
2  Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na 
nani katika ukuu wako?
3  Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na 
kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana.
4  Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche 
yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni.
5  Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake 
viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza.
6  Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao katika vitanzu vyake, na chini ya 
matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa 
makuu yote walikaa.
7  Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana 
mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi.
8  Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa kama vitanzu 
vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo 
wote uliofanana naye kwa uzuri.
 9  Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, 
iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu.
 10  Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele 
chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake;
 11  mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda 
mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake.
 12  Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya 
milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika 
karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika 
uvuli wake na kumwacha.
 13  Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani 
watakuwa juu ya matawi yake;
 14  kusudi mti wo wote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, 
wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo 
chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za 
chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.
 15  Bwana MUNGU asema hivi, Katika siku ile alipotelemka mpaka kuzimu naliamuru 
matanga, nalikifunika kilindi kwa ajili yake, nikiizuia mito yake, nayo maji makuu 
yalizuiwa; naliamuru Lebanoni kumwombolezea, na miti yote ya kondeni ilizimia kwa 
ajili yake.
 16  Niliwatetemesha mataifa kwa mshindo wa kuanguka kwake, hapo nilipomtupa chini 
mpaka kuzimu, pamoja nao washukao shimoni; na miti yote ya Adeni, miti iliyo miteule 
na iliyo mizuri ya Lebanoni, yote inywayo maji, ilifarijika pande za chini za nchi.
 17  Hao nao walitelemka kuzimuni pamoja naye kwa watu waliouawa kwa upanga; naam, 
wale waliokuwa mkono wake, waliokaa chini ya uvuli wake kati ya mataifa.
 18  Umefanana na nani, hivi katika utukufu na ukuu, kati ya miti ya Adeni? Lakini 
utashushwa pamoja na miti ya Adeni, hata pande za chini za nchi; utalala kati ya hao 
wasiotahiriwa; pamoja na hao waliouawa kwa upanga. Huyu ndiye Farao, na jamii yote ya 
watu wake, asema Bwana MUNGU.