Mithali
Mlango 16
1 Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.
2 Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huzipima roho za watu.
3 Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.
4 Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.
5 Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu.
6 Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu.
7 Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye.
8 Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.
10 Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme; Kinywa chake hakitakosa katika hukumu.
11 Mizani ya haki na vitanga vyake ni vya Bwana; Mawe yote ya mfukoni ni kazi yake.
12 Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo; Maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki.
13 Midomo ya haki ni furaha ya wafalme; Nao humpenda yeye asemaye yaliyo sawa.
14 Hasira ya mfalme ni kama wajumbe wa mauti; Lakini mtu mwenye hekima ataituliza.
15 Kuna uhai katika nuru ya uso wa mfalme, Na fadhili zake ni kama wingu la masika.
16 Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.
17 Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.
18 Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.
19 Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.
20 Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye Bwana ana heri.
21 Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara; Utamu wa maneno huongeza elimu.
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao; Bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao.
23 Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake.
24 Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani.
25 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
26 Nafsi yake mfanya kazi hujifanyia kazi; Maana kinywa chake humtia bidii.
27 Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao.
28 Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki.
29 Mtu mkali humshawishi mwenzake; Humwongoza katika njia isiyo njema.
30 Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; Aikazaye midomo yake hutokeza mabaya.
31 Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki.
32 Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.
33 Kura hutupwa katika mikunjo ya nguo; Lakini hukumu zake zote ni za Bwana.